
credit: nakupaushauri blog
Wataalamu
wa masuala ya mapenzi wanasema kuna aina nyingi sana za mapenzi
miongoni mwa binadamu. Hivyo ni muhimu kufahamu kuwa kupenda kwa mtu
mmoja au watu kadhaa hakuwezi kulinganishwa na wengine kwa mazingira na
mienendo.
Wakati fulani niliwahi kufanya uchunguzi miongoni mwa
wapenzi ambapo nilikuwa nawauliza swali. “Vipi dada/ kaka, huyu ni
mpenzi wako?” Wengi kati ya niliowauliza hawakupoteza hata nusu sekunde
kujibu ‘NDIYO’.
Lakini watu hao hao nilipowauliza kwa mara
nyingine “Unampenda kwa sababu gani?” Majibu ya wengi yalikuwa na sababu
ambazo si za msingi na wengine walinyamaza au kuambulia kucheka.
Hebu
wakati tunaendelea na mada hii, jiulize wewe mwenyewe ambaye una
mke/mume swali kama hilo unampendea nini huyo mpenzi wako? Baada ya hapo
sababu zinaweza kuwa ni kama zifuatazo “ Nampenda kwa sababu ni mzuri
wa sura, tabia, umbo, na kusema kweli ananivutia” la kama hizo
hazitakuwa sababu sina shaka nawe utanyamaza au utacheka.
Hii ina
maana kuwa watu wengi ambao tuna wapenzi iwe wake au waume zetu, huenda
tuliwapenda au tunawapenda hadi sasa bila kufahamu kwa nini tunawapenda
na kitu gani kilitufanya tuwe wapenzi. Maana ikiwa ni uzuri, tabia,
mvuto na sababu nyinginezo, basi lazima tufahamu kuwa uhai wa mapenzi
yetu ni mdogo.
Inasemwa hivyo kwa sababu watu hubadilika tabia,
sura, umbo, mvuto, ufahamu na hivyo kuweka ukomo wa mapenzi kuwa ni
baada ya kutokea kwa mabadiliko hayo ambayo ni ya kawaida katika maisha
ya mwanadamu, kwani ni wazi kwamba hakuna kinachodumu miongoni mwa hivyo
vinavyotajwa na wengi kama sababu za kupendana.
Watalaam wa
elimu nafsi na hasa Bw. Robert Stenberg walijitahidi sana kufanyia
utafiti wa mapenzi na kuibuka na aina kuu kiasi cha nne ambazo
wanazitaja kuwa ni PENZI LA UTIIFU, PENZI LA KUJALIANA, PENZI LA
UIGIZAJI NA PENZI TIMILIFU.
Ufafanuzi unaotolewa na wataalamu
hawa unaonyesha dhahiri makosa yanayoweza kufanywa na binadamu katika
kuchagua au kupata wapenzi. Jambo ambalo limepelekea kuporomoka kwa
uhusiano mwingi kati ya wanaume na wanawake. Wanasema penzi kamili
linatakiwa kuwa na sifa tatu, ambazo ni tendo la ndoa, ukaribu na
kujitolea.
PENZI LA UTIIFU
Penzi la utiifu au kama wengi
wanavyolifahamu hujulikana kama ‘penzi la mahaba’. Katika aina hii ya
penzi, wanaopendana hujali sana na kuendekeza zaidi miito ya kimwili.
Mapenzi ya kiwango cha juu kabisa miongoni mwao hupatikana pale
wanaposhiriki tendo la ndoa. Pia wanaopendana hupenda kuwa pamoja au
karibu kwa muda mwingi.
Lakini kwa bahati mbaya penzi la aina hii
linakosa sifa moja ambayo ni kujitolea. Wapenzi kwenye penzi hili
huonekana na pengine hujiona kuwa wanapendana, lakini unapofika wakati
ambapo kujitolea kunahitajika, penzi lililoonekana kushamiri hupukutika
ghafla.
Kujitolea kunaweza kuwa na maana ya kuumia kwa ajili ya
mwingine, kutoyumbishwa na watu wa pembeni na kuwa tayari kulinda penzi
hilo kwa gharama yoyote. Kwa mfano ukiona mpenzi wako hayuko tayari
kukusaidia unapoumwa, unapokuwa na matatizo, hakuhurumii unapokuwa
taabuni ujue kuwa mapenzi yenu ni ya utiifu ambayo uhai wake ni mdogo.
Jambo
la kufanya hapa ni kwa wapenzi wenyewe kujitambua na kuchukua hatua za
kukamilisha pengo la kujaliana ili kutowapa nafasi wambea na shida za
dunia kuyumbisha meli ya penzi ambayo wanasafiria, ikishindikana watu
hawa wanashauriwa kutokuwa wepesi wa kuoana kwani uwezekano wa ndoa yao
kutodumu ni mkubwa.
PENZI LA KUJALIANA
Penzi la kujaliana
ni lile ambalo wanaopendana wanakuwa karibu mara zote na kushiriki mambo
mengi pamoja. Wapenzi wa kundi hili huwa na hali ya kujitolea tofauti
na penzi la utiifu ambalo tumeliangalia, lakini kasoro yao kubwa huwa
kwenye miito ya mwili. Jambo la kufurahisha hapa ni kwamba wapenzi wa
kundi hili wako makini kwa kila sehemu na mara nyingi huwa hawakubali
kuingiliwa maamuzi ya mapenzi yao.
Lakini linapokuja suala la
tando la ndoa hujitokeza kasoro nyingi za kutofikishana kileleni au
kutofurahishana na hivyo anguko lao huletwa na muwasho wa mwili ambao
huwasukuma wapendanao hao kutoka ndani ya uhusiano wao na kufanya
usaliti.
Sasa ili kulifanya penzi la aina hii liwe imara lazima
wapenzi waulizane kuhusu kutimiziana haja za mwili wanapokuwa faragha.
Kama kuna kasoro kati yao si busara kufichana wanatakiwa kuwaona
wataalamu wa mapenzi na kupata ushauri utakaosaidia kuondoa tatizo hilo.
Hawa pia wanashauriwa kutooana haraka.
PENZI LA UIGIZAJI
Penzi
la aina ya tatu linalotajwa na watafiti ni lile lijulikanalo kama penzi
la Uigizaji. Hili ni lile penzi ambalo wanaopendana hukutana asubuhi na
ikifika jioni tayari ni wapenzi kamili, ambapo hugandamana kama ruba,
utadhani waigizaji wako kwenye matayarisho ya filamu. Ukiwatazama
wanakuwa kama vichaa na msukumo wao wa kutimiza hisia za mwili huwa ni
mkubwa kiasi cha kufikia kufanya mapenzi hata barabarani au kwenye
sehemu za wazi.
Wapenzi wa aina hii huchukua muda mfupi sana
kutangaziana mambo ya ndoa na pengine kuoana bila kufahamiana zaidi
kitabia. Wanajuana asubuhi na jioni mwanamke/mwanaume keshahamia kwa
mwenzake na maisha yanaanza, hapo hakuna ushauri wala muongozo wa watu
wengine.
Tatizo kubwa ambalo hujitokeza katika penzi la aina hii
ni wapenzi kuchokana mapema na hamu ya kufanya tendo la ndoa kupotea.
“Yaani nikiwa na mume wangu sijisikii kabisa kufanya naye mapenzi,
lakini kwa wengine nakuwa na hamu sana” hizi ni kauli za wapenzi wa
penzi la kisinema sinema.
Mbali na hilo wapenzi wa aina hii ni
rahisi kuporwa na kuanzisha uhusiano mpya, hivyo inashauriwa kuwa kwa
wale ambao wanaona kuwa wako kwenye kundi hili, wajitahidi kujizuia na
kupeana nafasi za kujuana zaidi kupitia ushauri wa watu wengine. Si vema
kushiriki tendo la ndoa kila mara kwa staili na sehemu zile zile na pia
haifai kukurupuka kuoana bila kuchunguzana tabia, ndoa za hivi
hazidumu.
PENZI TIMILIFU
Aina ya mwisho ya penzi kama
inavyoelezwa na mtaalamu Sternberq ni ile ya penzi timilifu. Aina hii ya
mapenzi inakuwa na sifa zote tatu, yaani TENDO LA NDOA. Kwamba
wapendanao huwa hawana kasoro katika eneo hili, unapofika muda wa
kupeana raha hufikishana mahali pa juu. UKARIBU kwamba muda wote huwa
karibu na kila mmoja hakai na kiu ya kutokumuona mwenzake kiasi cha
kupoteza hisia na kushawishika kufanya usaliti.
Sifa ya mwisho ni
KUJITOLEA. Ni mahodari kusaidiana, kufarijiana na hawako tayari kupokea
mambo kutoka pembeni yanayohusu uhusiano wao, hivyo huwa si rahisi kwao
kuyumba kwa sababu za umbea. Kumbuka katika penzi hili tendo la ndoa
huwa si sehemu muhimu sana kwa wapenzi, yaani kwao penzi ni rohoni zaidi
kuliko mwilini hata wakikaa muda wa miezi mitano bila kufanya tendo la
ndoa upendo wao haupungui.
Hata hivyo, penzi la aina hii kwa
mujibu wa wataalamu ni vigumu kupatikana na ni vigumu pia kulilinda,
lakini linatajwa kuwa ni aina ya penzi bora ambalo ni muafaka kwa maisha
ya baadaye ya ndoa kwa wanaopendana. Watu wengi kwa kutotambua aina hii
ya mapenzi wamejikuta wakiliharibu kwa kufikiri tu kwamba wapenzi wao
wamefika na hivyo kufanya makusudi ya kuharibu misingi ya penzi.
“Nimeshamshika
atakwenda wapi, nikikohoa tu anaitika” Kauli kama hizi ni hatari sana
katika penzi hili, hivyo inashauriwa ukiona unapendwa na mpenzi wako
katika aina hii ya penzi ni vema ukawa macho ili kutolivunja kwa uzembe
wako na kudhani unababaikiwa kumbe unapendwa kwa dhati.