Serikali imesema inaangalia utaratibu wa watahiniwa
240,903 wa kidato cha nne waliopata daraja sifuri katika matokeo yaliyotangazwa
hivi karibuni, kurudia mtihani mwaka huu kwa gharama zake.
Aidha, imesema matokeo mabaya ya mwaka huu yamesababishwa
na mambo makuu manane, kubwa likiwa ni wanafunzi waliopita bila kuchujwa katika
mtihani wa kidato cha pili walioufanya miaka miwili iliyopita.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo
Mulugo alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu hatua
zitakazochukuliwa na Serikali kutokana na idadi kubwa (asilimia 60.6) ya
watahiniwa wa kidato cha nne kufeli mtihani wa Taifa kwa daraja sifuri na
hatima yao ya kujiuzulu.
Akifafanua, Mulugo alisema, “suala la kujiuzulu lipo nje
ya mipaka yangu ya kazi kwa kuwa halihusishi wizara moja wala Serikali pekee.
Lakini kuhusu hatua zitakazochukuliwa kwa waliopata sifuri, Serikali inafikiria
warudie mtihani mwaka huu”.
Ingawa alisema wazo hilo halijapitishwa, lakini hivi sasa
linajadiliwa kuona namna ya kuwasaidia watahiniwa zaidi ya 240,000 waliopata
alama hiyo, kurudia mtihani wa Taifa kwa gharama za Serikali. Watahiniwa
waliosajiliwa walikuwa 480,036.
“Katika kuchambua hilo, tumeangalia namna ya kuwalipia
ada ya mtihani ambayo mwaka jana walilipa Sh 35,000 kila mwanafunzi, likipita
hilo la kurudia mtihani, Serikali italipia ada hiyo na wataufanya kama
watahiniwa binafsi,” alibainisha Mulugo.
Sababu za kufeli
Kuhusu matokeo mabaya, Mulugo alisema sababu kubwa ni
kutokuwapo mchujo kwa watahiniwa waliopata chini ya asilimia 30 wakati
walipofanya mtihani wa kidato cha pili na hali hiyo inaweza kujitokeza hata kwa
watahiniwa wa kidato cha nne mwaka huu.
“Hawa ni waliofanya mtihani wakati mfumo wa kuwachuja
walipokuwa kidato cha pili ulikuwa umeondolewa, walipita wote, iwe alipata F au
A, na walipita kwa miaka miwili, hivyo hata mwaka huu athari zinaweza kutokea,
ila watakaoingia kidato cha nne mwakani, walichujwa na sifuri zilikuwa zaidi ya
136,000, hivyo tofauti inaweza kuwapo,” alifafanua.
Hata hivyo, alisema matokeo hayo mabaya hayatarekebishwa
kwa namna yoyote, ili kuongeza idadi ya watakaoingia kidato cha tano mwaka huu,
bali watahiniwa 23,500 waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ndio
watakaoendelea.
Alisema watakaochukuliwa Ualimu ni wa daraja la nne ya
alama 26 na 27 huku wenye alama 28 wakiachwa bila kuchukuliwa mwaka huu.
Kujiuzulu?
Akielezea shinikizo la kuwataka yeye, Waziri Dk Shukuru
Kawambwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce
Ndalichako wajiuzulu, Mulugo alisema suala hilo liko nje ya mipaka yake ya kazi
kwa kuwa linahusisha Wizara zaidi ya moja.
“Si sahihi kulizungumza hilo la kujiuzulu, kwa kuwa liko
nje ya mipaka yangu ya kazi, si suala la Wizara ya Elimu pekee, ni mtambuka na
linashughulikiwa na wizara zaidi ya moja, hata hivyo hatua tayari zinachukuliwa
kutafuta kwanza kiini cha tatizo na mpaka sasa tumegundua mambo manane.
Akiyataja, Mulugo alisema ni pamoja na jamii kutosaidia
wanafunzi kufikia malengo, wanafunzi wenyewe, mitandao ya kijamii nje ya
masuala ya elimu, wazazi, Sayansi na Teknolojia na Serikali katika mipango na
sera, mwingiliano wa uwajibikaji kitaasisi (wizara zaidi ya moja, ikiwamo
Tamisemi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu).
Kuhusu madai ya mtihani mgumu uliokuwa na mbinu za
kitaalamu zaidi, Mulugo alisema hakuna mtihani mwepesi duniani na kuongeza,
kwamba uwajibikaji wa wanafunzi katika elimu umefifia kutokana na uhuru mkubwa
walionao kupitia mitandao ya jamii na vyombo vya habari, huku akidai baadhi
wanaiga kwa kasi mabaya wanayoyaona humo na kuyahamishia katika mitihani.
Utungaji
Pia alieleza namna mtihani unavyotungwa na kubainisha,
kuwa Necta huandika barua kwa Ofisa Elimu wa Mkoa akiomba walimu makini walio
kazini, watunge maswali ya mwongozo wa mtihani na maswali hayo hupelekwa katika
Baraza na huko walimu baadhi kuyapitia tena.
“Baada ya hapo walimu angalau wawili au watatu kutoka
kila mkoa huweka kambi ya siku si chini ya 10 kuhakiki na kupitia maswali hayo,
kisha Necta huunda kamati ndogo inayapitia miongoni mwao maswali yanakuwa
mtihani na si nje ya hapo. Utaona anayetunga mtihani ni mwalimu anayemfahamu
mwanafunzi,” alisema Mulugo.
Katika kusahihisha, kwa mujibu wa Mulugo, walimu makini
kutoka kila mkoa huchukuliwa kwa uwakilishi na kupangiwa vituo vya kusahihisha
mtihani, na walimu wa somo moja hukaa kituo kimoja tofauti na wa somo lingine
na mwalimu mmoja husahihisha swali moja na kumpa mwenzake.
“Haiwezekani kumpendelea mtu, unakuta mtihani wa hesabu
uko Kilimanjaro, Kiingereza uko Dar es Salaam, labda wa Kiswahili unasahihishwa
Mbeya, sasa walimu wote wanakujua ama wakupendelee au kukuonea?”
Alisema na kusisitiza kuwa matokeo ya mwaka huu
yalitokana na udhibiti wa wizi wa mitihani uliofanywa na Serikali na utaendelea
miaka yote.
Aliitaka jamii kushirikiana kuwawezesha wanafunzi kufikia
malengo ya elimu kwa kudhibiti katika matumizi ya simu, mitandao ya jamii na
wizi wa mitihani na kuongeza kuwa suala la elimu linapaswa kuwa la wote, huku
Serikali ikiwa ni mtunga sera na msimamizi.
Yamekuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa kada
mbalimbali kuhusu kufeli kwa kiasi kikubwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne
mwaka jana.
Post a Comment