SERIKALI imelipa mishahara hewa zaidi ya Sh400
milioni kwa watumishi ambao hawapo kazini Hospitali ya Enduleni, Wilaya
ya Ngorongoro, mkoani Arusha kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi
kwenye hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Katoliki Jimbo la
Arusha, umebaini takribani tangu mwaka 2009 hadi sasa, serikali imekuwa
ikituma Sh8.2 milioni kila mwezi kulipa watumishi 13 ambao wameacha
kazi.
Watumishi hao majina yanahifadhiwa, wanadaiwa
kuacha kazi hospitalini hapo kutokana na kuzorota kwa huduma,
kulikochangiwa na upungufu wa dawa na kushindwa kulipwa stahiki
nyingine.
Hospitali hiyo ambayo ipo ndani ya Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro, imekuwa ikihudumia zaidi ya wakazi 70,000 wa
Tarafa ya Ngorongoro kutokana na eneo hilo kutokuwa na hospitali
nyingine.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Fransis Mwasangi
alikiri hospitali hiyo kupokea kiwango hicho tangu mwaka 2009 kwa
watumishi wasiokuwapo kazini.
Hata hivyo, Dk Mwasangi alisema tayari ofisi yake
imepeleka taarifa serikalini kuhusu hali hiyo na kuomba majina ya
watumishi hao, kuondolewa na kuingizwa mengine 13 lakini suala hilo
halijafanyika.
“Ingawa siyo msemaji wa hospitali, lakini ni kweli
tatizo hili lipo binafsi na wenzangu tumepeleka majina serikalini mara
kadhaa ya watumishi wapya na vyeti vyao, lakini hawajaingizwa kwenye
orodha ya malipo,” alisema Dk Mwasangi.
Alisema tatizo la kuendelea kupelekwa mishahara ya
watumishi ambao hawapo, linazikabili hospitali nyingi nchini hasa
kutokana na kutokufanyika kwa mapitio ya mishahara.
“Tuliamua fedha hizi zinazokuja hapa tuzitumie kuwalipa watumishi tulionao kwani wana sifa,” alisema.
Licha ya kuondoka watumishi hao, hospitali hiyo
inakabiliwa na ukata na kushindwa kuwalipa mishahara watumishi wengine
wanaodai Sh20 milioni kwa miezi sita sasa.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya (Tughe)
hospitalini hapo, Christopha Bajuta alithibitisha kutolipwa wafanyakazi
kadhaa na kwamba, tayari wametoa malalamiko kwa bodi ya hospitali.
Awali, Mhasibu mkuu wa hospitali hiyo, Damas Mapunda alikiri kupokea Sh8.2 milioni kila mwezi kwa watumishi ambao hawapo.
“Kweli tunapokea hizo fedha lakini tunazitumia kulipa wengine, tatizo ni serikali siyo sisi,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari wametoa taarifa Serikalini kuhusu kuondoka kwa watumishi hao na wengine ambao wamepatika, lakini serikali imekaa kimya.
“Kweli tunapokea hizo fedha lakini tunazitumia kulipa wengine, tatizo ni serikali siyo sisi,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari wametoa taarifa Serikalini kuhusu kuondoka kwa watumishi hao na wengine ambao wamepatika, lakini serikali imekaa kimya.
MWANANCHI
Post a Comment