MAHAKAMA ya Mwanzo mjini hapa, imemtia hatiani aliyekuwa mtawa wa Shirika la Kitawa la Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga, Sista Yasinta Sindani, kwa kufumaniwa na mume wa mtu na kuamriwa kumlipa fidia ya Sh 700,000 mlalamikaji.
Katika kesi ya msingi ya madai, mlalamikaji Asteria Mgabo alimtaka Sista Yasinta amlipe Sh milioni 3 baada ya kumfumania na mumewe wa ndoa, Martin Msangawale (39) ambaye pia ni mkazi wa mjini hapa.
Sista huyo ambaye ni daktari katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa, kwa sasa anaishi nje ya nyumba ya utawa eneo la Kantalamba.
Katika hati ya awali ya madai, inadaiwa mshitakiwa alifumaniwa na Asteria akiwa na mumewe Msangawale wakiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Chipa iliyopo eneo la Katandala mjini hapa, Desemba 24 mwaka jana majira ya saa 7 usiku ikiwa ni siku ya mkesha wa Sikukuu ya Krismas.
Akisoma hukumu hiyo juzi, hakimu wa mahakama hiyo, Jaffar Mkinga alisema kuwa ushahidi uliotolewa na mlalamikaji ulikuwa mzito wenye kuondoa shaka zote kuwa mdaiwa alitenda kosa hilo tofauti na utetezi uliotolewa na mdai kuwa ulikuwa dhaifu.
Awali katika utetezi wake mdaiwa aliiambia mahakama hiyo kuwa kwanza alikuwa hajui kuwa Martin alikuwa mume wa mtu na kukiri mbele ya mahakama hiyo kuwa alimweleza kuwa hana mke hivyo alimwomba amuoe.
Lakini Hakimu Mkinga alipinga utetezi huo kwa sababu usiku huo wa mkesha wa Krismas mwaka jana, saa saba na robo usiku, mlalamikaji akiongozana na mwenyekiti wa mtaa wakiwa na mashahidi wengine watatu, walimkuta mdaiwa na Martin wakitoka katika moja ya vyumba katika nyumba ya kulala wageni ya Chipa, akasainishwa.
“Kama hukufahamu kuwa Martin alikuwa hana mke ilikuwaje ukakubali kusaini karatasi hiyo ya fumanizi iliyoandaliwa na mwenyekiti huyo?” alihoji hakimu, akamhukumu kulipa sh 700,000.
Post a Comment