Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton,
anatarajiwa kufika mbele ya bunge la Congress kujieleza kuhusu mashambulizi
mabaya yaliyofanywa dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya, mwaka
jana.
Bi Clinton atakabiliwa na maswali kutoka kwa kamati za bunge la Senate na la
waakilishi kuhusu maswala ya kigeni, juu ya usalama mbovu uliosababisha
mashambulizi hayo.Balozi wa Marekani nchini Libya Christopher Stevens pamoja na maafisa wengine watatu wa ubalozi huo, waliuawa kwenye mashambulizi hayo.
Balozi huyo alifariki kutokana na moshi wakati aliponaswa ndani ya jengo lililokuwa linateketea.
Hii ni baada ya wapiganaji wa kiisilamu kuvamia ubalozi.
Mashambulizi hayo yalisababisha mvutano wa kisiasa swali likuwa nani aliyekuwa na taarifa kuhusu shambulizi hilo.
Kwa kuwa Clinton ni mwanachama wa Democrat ambao wanadhibiti bunge la Senate, atakuwa anahojiwa kwa njia ya heshima lakini atakabiliwa na wakati mgumu kutoka kwa wabunge wa bunge la waakilishi ambao wengi ni wanachama wa Republican.
Jopo hilo huenda lisimlimbikizie lawama sana Clinton kwa utovu wa usalama kwenye ubalozi huo, lakini wanachama wa Congress bado watataka kujua kwa nini hakuwa na taarifa kuhusu ombi la kuimarisha usalama katika ubalozi huo.
Pia atakabiliwa na maswali kuhusu ambavyo serikali ya Obama ilishughulikia mzozo huo.
Wafanyakazi watatu wa serikali walifutwa kazi kuhusiana na shambulizi la Benghazi na mapendekezo yaliyotolewa na jopo hilo mwezi Disemba tayari yanashughulikiwa.
Post a Comment