Games

LATEST UPDATES

Sunday, January 27, 2013

Baada ya vurugu kubwa Dumila, hali bado tete wilayani Kilosa…


Hali bado ni tete katika baadhi ya vijiji wilayani Kilosa, Morogoro baada ya kutokea kwa vurugu kubwa kati ya wakulima na wafugaji wa eneo la Dumila wilayani humo.

Taarifa zilizoifikia FikraPevu kutoka wilayani Kilosa zinaeleza kwamba pamoja na polisi kutuliza ghasia mapema leo asubuhi, kuna taarifa za ulipizaji visasi katika maeneo mengine wilayani humo baada ya wafugaji wengi wakiwa wenye asili ya Kimasai kuharibiwa mali zao katika vurugu za awali.
"Unajua watu hawa (wakulima) waliharibu mali za wananchi wenzao hasa wenye asili ya Kimasai ikiwamo kuvunja nyumba zao na gari moja, sasa kuna hofu ya ulipizaji kisasi maeneo mengine," anasema mtoa habari aliyeko Dumila.
Watu wanaojitambulisha kama wakulima walifunga barabara na kuanza kupiga mawe magari na baadaye kuvamia nyumba za wananchi wenzao na kuliharibu gari moja linaloelezwa kuwa la mfugaji wa Kimasai.
Wananchi wanaohusishwa na vurugu hizo wanadai kwamba uongozi wa wilaya ya Kilosa chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Elias Kimario, umegawa kwa wafugaji maeneo yao ya kilimo na hivyo walitaka kusikia kauli ya uongozi wa mkoa.
Hata hivyo, taarifa kutoka wilaya za Kilosa na Mvomero zinaeleza kwamba chanzo cha vurugu hizo ni vuguvugu la kisiasa miongoni mwa wananchi hao na hivyo kupinga kauli ya Mkuu wa Wilaya kwamba eneo husika kisheria lilitengwa kwa ajili ya wafugaji pamoja na kuwa lilikuwa likitumika kwa kilimo.
"Kwanza unajua hata vurugu zenyewe kutokea katika siku ya mapumziko ni kwa sababu wahusika wakuu wanaochochea vurugu hizo wanatoka nje ya Kilosa ikiwamo Arusha, Dar es Salaam na Morogoro mjini. Tumeshaamua Tanzania kila kitu tunafanya siasa," anaeleza Ofisa Mmoja wa Serikali mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, Jeshi la Polisi limeongeza nguvu kwa kuchukua askari zaidi kutoka Mvomero na Morogoro kulinda hali ya usalama baada ya ghasia za mapema leo kutulizwa.
Awali, mdau katika JamiiForums aliripoti uwepo wa vurugu hizi na wananchi walikuwa wakitoa taarifa kadiri muda ulivyokuwa ukiruhusu kitendo kilichoilazimu FikraPevu kufuatilia kwa ukaribu kufahamu chanzo cha vurugu na hatua gani mamlaka husika zimechukua.
Share This :

Post a Comment

 

Top