Msichana aliyebakwa |
Mtu anayesadikiwa kuwa muumini wa kiislam Ahamad Fadhili (63), amenusurika kuuawa kwa kipigo, akihusishwa na jaribio la kubaka ndani ya msikiti.
Tukio hilo limetokea katika msikiti wa Mwembe Mmoja uliopo Ujiji, mkoani Kigoma na kushuhudia na umati wa watu wakiwamo waumini wa msikiti huo.
Fadhili anadaiwa kujaribu kumbaka msichana wa umri wa miaka 24 (jina tunalihifadhi), anayesumbuliwa pia na ugonjwa wa kifafa.
Vyanzo kadhaa vya NIPASHE Jumamosi katika eneo hilo, vilieleza kuwa katika tukio hilo la Februari 19, mwaka huu, majira ya saa nane mchana, Fadhili alikutwa akimbaka msichana huyo ikiwa ni baada ya swala ya adhuhuri.
Mrekwa Kabichi, muumini katika msikiti huo alisema, baada ya kuswali, alimuona kiongozi wa msikiti huo, akimtaja kwa jina la Mzee Sande, akitoka ndani ya msikiti huku akifoka.
“Tukamuuliza, kuna nini mbonaunafoka, kasema nimemkuta Ahamad Fadhili akimbaka binti ndani ya msikiti wetu, tukamuuliza wako upande gani akatwambia ni yule ambaye anakimbia,” alisema.
Aliongeza, “tukamkimbiza hadi kumkamata, tukampa kipigo kisha tukampeleka kituo cha polisi kati ili sheria ichukuwe mkondo wake.”
Imamu wa msikiti huo, Shabani Hashimu Juma, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa kitendo hicho kimeisikitisha jumuiya ya waislamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wanamshikilia mtuhumiwa huyo na kwamba atafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.
NIPASHE Jumamosi ilienda hospitali ya mkoa, Maweni katika wodi namba tano, na kumkuta msichana huyo akiwa amelazwa.
Msichana huyo alisema siku ya tukio, majira ya saa saba mchana, alienda msikitini hapo kuomba msaada, kwa vile anaugua kifafa.
“Nilipofika, nilikutana na huyo baba akaniambia ni kiongozi wa msikiti, hivyo nimsubiri akanichangie fedha kwa waumini,” alisema.
“Ndipo mimi nikaingia ndani ya msikiti, upande wa wanawake kuswali, baada ya kumaliza mzee huyo aliniita na kuniingiza ndani ya eneo jingine nikafikiri naenda kuchukua mchango, kumbe naenda kubakwa,”aliongeza.
Alidai kuwa mtuhumiwa alimpapasa, na kwamba alijitahidi kukataa, lakini ‘aliishiwa nguvu’ hivyo kutoa fursa ya kuangushwa chini na kubakwa.
Kwa mujibu wa msichana, wakati tukio hilo likiendelea, alitokea mzee mwingine (Sande) na kuwatenganisha.
“Alimtoa juu yangu na huyo baba (mtuhumiwa) kuanza kukimbia, ndipo waumini wa msikiti walimkimbiza na kumkamata na kuanza kumpiga,” alidai.
Alisema wakati huo, alikuwa amezimia na kwamba alipozinduka alijikuta akiwa wodini hapo.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Maweni, Yakayashi Macrice, alithibitisha kupokea mgonjwa aliyebakwa, ikielezwa kwamba tukio hilo lilitokea msikitini.
Alisema msichana alipata matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Source:Nipashe
Post a Comment