Games

LATEST UPDATES

Monday, February 18, 2013

MAKUNDI YA WANAUME NA MITAZAMO YAO YA KIMAPENZI KWA WANAWAKE -4

LEO tunaanzia pale tulipoishia wiki iliyopita kwa kuanza kuchambua kundi la pili. Kimsingi, kuna wanaume ambao hawajui kushukuru hata wafanyiwe kitu gani. Hawa ndiyo wanaunda kundi hili la pili ambalo linatokana na wale wenye tabia ya kutazama masilahi kwanza kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Unaweza kushangaa mtu anakutana na warembo ambao wapo singo lakini hajishughulishi nao, badala yake anapoona wake za watu akili inamtoka. Tatizo kubwa lililopo ndani yake ni kwamba anakimbia majukumu. Hawezi kuhudumia.
Atatokea mrembo anayetazamika hasa. Atampa mapenzi yote lakini hataridhika kwa hilo. Atakachokifanya ni kuhamishia uhusiano wake kwa mwanamke mwenye fedha ili apate kuchota noti za benki kuu. Siku zote ni wasafi na hujiweka kwenye muonekano wa kati.
Si kila mke wa mtu anaweza kumtolea macho. Kuna vipimo huvizingatia, kama vile anapomuona mwanamke anaendesha gari, pengine amechakaa madini shingoni na mikononi na kadhalika. Hapo hujiridhisha kuwa mwanamke husika siyo mtu wa shida.
Ni kweli kwamba akili zao huzikita kwenye mapenzi na wanawake watu wazima, wafanyabiashara au wake za watu ambao wanaonekana kuwa na pesa, hata hivyo wanaweza kujiweka kwenye mapenzi na wanawake vijana wenye kujitafutia.
Kwa vile mwanamke mwenyewe anakuwa anahangaika na maisha, hawezi kuwa na kiasi kikubwa cha fedha kumridhisha mwanaume mwenye sifa zinazomfanya aunde kundi hili. Kutokana na hali hiyo, mwanaume husika hatatulia kwa maana hana shukurani.
Mara nyingi, wanaume wa kundi hili, huwaacha wanawake wakiwa katika maumivu makali. Wanaweza kuonekana bora zaidi kwenye uhusiano wa kimapenzi wakati wa kuanza lakini baadaye hubadilika. Tena hubadilika ghafla.
Unaweza kukutana na mwanamke ambaye hajui kisa cha mpenzi wake kumbadilikia. Atasimulia yote waliyofanya pamoja na namna ya pekee alivyokuwa akimjali na kumpa mapenzi yenye uzani wa juu, mwisho atasema: “Sasa nashangaa ghafla tu kanibadilikia.”
Kisaikolojia, mwanaume mjenzi wa kundi hili anapofanya makosa ambayo yanalalamikiwa na mwanamke (wanawake), huwa hajielewi. Kiburi  na tamaa ya kupata mahitaji yao, huwafanya wawe vipofu pale wanapowatenda wenzi wao.

TATHMINI KIMAPENZI
Wanaweza kuangukia hata kwa wanawake wasiowapenda ilimradi wapate unafuu wa kuishi vizuri. Wao huwa hawana kile kitu kinachoitwa ‘mapenzi ya dhati kutoka moyoni’, wao ni waumini wakubwa wa ule mtindo wa kula na kuondoka. Uzuri wa mwanamke na kiwango cha pesa humfanya adumu.
Kutokana na ukweli huo kwamba huwa hawazingatii mapenzi ya dhati kutoka moyoni, wanaume wanaounda kundi hili wakati mwingine huwa hawachagui umri wa wanawake kabla ya kuanzisha nao uhusiano. Iwe ni kwa vijana wadogo mpaka wazee wenye umri sawa na vikongwe.
Kijana mwenye umri wa miaka 24, anapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mama mwenye umri wa miaka 40 au 50 ambaye kiuhalisia ni sawa na mzazi wake, hilo haliwezi kuwa jambo geni, isipokuwa kilichozingatiwa na mwanaume husika ni unafuu wa kuishi.


Share This :

Post a Comment

 

Top